Popis: |
Madhumuni ya makala haya ni kujadili maudhui yanayojitokeza katika bembelezi za wanawake Watikuu nchini Kenya ili kutambua ujumbe uliyomo. Kwa muda mrefu, kitanzu cha bembelezi cha nyimbo za watoto kimepuuzwa miongoni mwa watafiti nchini Kenya na barani Afrika kuna tafiti chache za kitanzu hiki zinazojulikana na watafiti. Bembelezi za wanawake Watikuu zina maudhui ya kipekee yanayotilia shaka hadhira yake na hili ndilo jambo lililowavutia waandishi wa makala haya kuzitafiti na kujadili maudhui yaliyomo. Utafiti wa awali uliofanywa na waandishi ulionyesha kwamba lugha inayotumiwa kuwasilisha ujumbe uliyomo ina urejelezi, kejeli na mafumbo chungu nzima ambayo ni kinyume cha sifa za lugha ya nyimbo za watoto. Mbinu za uteuzi wa kimaksudi na kuelekezwa zilitumiwa kuteua sampuli ya wasailiwa wa kike kumi na wanne wenye umri wa miaka katika 30-70 walioshirikishwa katika utafiti. Vikundi lengwa viwili viliundwa kutokana na sampuli hiyo. Kila kimoja kilijumlisha wasailiwa sita, cha kwanza kilikuwa na wasailiwa wenye umri kati ya miaka 50-60 na cha pili kilikuwa na wasailiwa wenye umri kati ya 30-48. Wasailiwa wawili wenye umri zaidi ya 64 walishirikishwa katika mahojiano ya kina. Bembelezi 20 zilikusanywa katika vikundi lengwa vya mjadala na sita zikateuliwa kimaksudi kwa misingi ya maudhui zilizobeba ili kutafitiwa. Matokeo ya utafiti huu yalionyesha kwamba, maudhui ya bembelezi za wanawake Watikuu hulenga si watoto tu, bali watu mbalimbali katika jamii hiyo. Lililodhihirika ni kwamba wanawake Watikuu hutumia bembelezi kama jukwaa la mawasiliano. Wanapowabembeleza watoto kwa kuwaimbia, huwa wanayatoa yaliyo mioyoni mwao kwa nyimbo hizo. |