Popis: |
Uhusiano baina ya lugha na utamaduni, mila na mirathi ya jamii kwa jumla huenda ukafahamika angalau kwa wepesi, iwapo tutazingatia mambo mawili: kwanza, lugha na matumizi yake ni chombo cha kujieleleza thamani tafauti zilizofungamana na maumbile ya kimila, fikira, maarifa, imani, adabu na utamaduni wa jamii yenyewe kwa jumla. Pili, matumizi ya lugha aghlabu husadifu kuwa ndio msingi wa kuendeleza na kukuza, na hata pia kubuni, uzushi mpya katika mirathi ya utamaduni, mila na khulka za kijamii. Kwa hivyo si rahisi kwa lugha kutengamana na taswira za jamii: utu, utamaduni, mila, mitindo na mengineo. Tungependa kuandaa madhumuni yetu ya kuonesha athari na hatari zinazokabili hali ile ya kutumia lugha geni katika kuendeleza shughuli za jamii au taifa la kienyeji. Muhimu pia, tutashughulika na athari za mtindo huo katika fasihi za kienyeji, hasa tunapozingatia kuwa fasihi ya maandishi ni mfano wa kioo cha hakika ya jamii. |